Jumapili , 4th Dec , 2022

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amelitaka Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma kuwakamata wafugaji wanaoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kuwachukulia hatua za kisheria.

Amesema haridhishwa na kasi ya Jeshi hilo katika kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji Mkoani humo ambapo matukio ya wafugaji yakuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima yanaongezeka na kusababisha uharibifu wa mazao kutokana na askari kutofanya wajibu wao ipasavyo.

Masauni ametoa kauli wakati akizungumza na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Wizara yake, Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma, wakati alipofanya ziara ya siku moja kutatua mgogoro wa wakulima na Wafugaji mkoani humo.

“Kazi yenu Polisi ni kulinda raia na mali zao, lakini bado hamnifurahishi katika kushughulika na migogoro ya wakulima na wafugaji, wananchi wametumia muda mrefu kuandaa mazao yao kwa ajili ya chakula na pia biashara ambapo watakapouza mazao hayo nchi itafaidika kwa kupata kodi, lakini wanatokea baadhi ya wafugaji wanaingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kufanya uharibifu mkubwa, hii haiwezekani katika Serikali ya awamu ya sita ambayo inataka haki,” alisema Masauni.