Jumanne , 1st Dec , 2020

Mbunge wa viti maalum kupitia CHADEMA,Halima Mdee, amesema kuwa hawezi kusema ni nani aliyepeleka majina yao Bungeni na wala ni kwanini waliapa, kwa kuwa hataki kuweka mambo hayo hadharani na badala yake ataenda kuyazungumza ndani na viongozi wa chama chake.

Halima Mdee na wenzake wakati wakizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Disemba 1, 2020, wakati wa mkutano wake na wabunge wenzake walioapishwa hivi karibuni, ambapo amesema kuwa yeye na wenzake kuanzia sasa ni wana CHADEMA wa hiyari na wala hawana mpango wa kuondoka ndani ya chama hicho kwa sababu wametoka nacho mbali.

"Kamati kuu imefanya uamuzi wake, tumesema tunaenda kukata rufaa baraza kuu, hizi hoja mbili ya kwanini tumeenda kuapa, au nani amepeleka majina ndiyo msingi wa rufaa zetu, siwezi kujadili hapa content , ndiyo maana nilisema kuna maswali nitayajibu na sitoyajibu tutaliongea ndani ya chama kwa sababu kila mtu ameshasema la kwake na hili ndiyo msingi mkuu wa kesi yetu", amesema Halima Mdee.

Aidha Mdee ameongeza kuwa, "Mimi sina dhamira ya kuondoka CHADEMA na hapa kila mmoja ameijenga CHADEMA kwa jasho na damu yake pamoja na changamoto tunazopitia maana hii wiki moja ilikuwa ya makashikashi kweli, niwahakikishie Halima mnayemfahamu miaka yote ndiyo yuleyule".