Jumatatu , 10th Jul , 2017

Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiangi, ametangaza amri ya kutotembea usiku kwa miezi mitatu katika County za Lamu, Tana River na Garissa ambazo zimekuwa zikishambuliwa mara kwa mara na wanamgambo wa Al – Shaabab.

Amri hiyo imetangazwa baada ya Bw. Matiangi kukutana na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa kikao cha Baraza la Taifa la Usalama la nchi hiyo.

Amri hiyo itaanza kutekelezwa mara moja kuanzia saa 12:30 jioni mpaka saa 12:30 asubuhi katika County hizo tatu na maeneo ya jirani ambayo yanaonekana kuwa hatari.

Hata hivyo, Bw, Matiangi, amesema amri hiyo haitahusu visiwa vya Lamu, Manda na Pate.

Siku ya Ijumaa usiku, watu tisa waliuwawa kwa kuchinjwa na wanamgambo wa Al – Shaabab katika vijiji vya Jima na Poromoko katika County ya Lamu, ambapo siku ya Jumatano wanamgambo hao walivamia kituo cha polisi na kuwaua maafisa watatu.