Jumatano , 13th Sep , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali za kisheria dhidi yake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Bw. Mousa Farhang jijini Dar es Salaam.

"Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu. Nawaomba wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha amani yetu. Kwa sasa serikali ipo katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na wahujumu uchumi", amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema licha ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.

"Mbali ya kuimarisha amani nchini, pia serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija. Hivyo natumia fursa hii kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili mje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo  vya kuchakata mazao ya  kilimo", amesisitiza Majaliwa.

Kwa upande wake, Balozi Farhang  ameipongeza serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.

Balozi huyo amesema serikali ya Irani ipo tayari kushirikiana na serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na vitendo vingine vya kihalifu.