Alhamisi , 27th Oct , 2016

Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa inakabiliwa na maombi makubwa ya mikopo kutoka katika halmashauri zake hadi kufikia shilingi bilioni 48.8 ikilinganishwa na shilingi bilioni 9.2 zinazotolewa sawa na asilimia 18.9.

George Simbachawene - Waziri wa TAMISEMI

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya mikopo mjini Dodoma leo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene, amesema, upo umuhimu wa kuangalia namna bora ya kuongeza mtaji ili kuboresha huduma ya bodi hiyo.

Mh. Simbachawene amesema ili kukabiliana na changamoto hizo lazima baadhi ya hatua zianze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na halmashauri  zinazodaiwa kutakiwa kulipa madeni kupitia makato ya benki.

Amesema halmashauri zitakazoidhinishiwa mikopo lazima marejesho yake yafanyike kulingana na makubaliano ya mkataba uliopo huku akiitaka bodi mpya kuhakikisha marejesho yanafanywa kwa wakati.

Pia Simbachawene aliwakumbusha majukumu wajumbe wa bodi ya mikopo kuwa pamoja na kuwajibika kuzisaidia halmashauri kutimiza malengo yao pamoja na upelekaji madaraka na majukumu zaidi kwa wananchi ambako kunahitajiwa fedha na nyenzo  zaidi za kufanyia kazi.

Amesema majukumu mengine ni umuhimu wa kuwezesha halmashauri kupata mapato ya ziada pamoja na kutoa msaada wa fedha kwa serikali za mitaa kwa njia ya ruzuku kwa niaba au faida ya serikali za mitaa.