Jumatano , 6th Jul , 2022

Moto mkubwa umezuka ghafla na kuteketeza moja ya bweni lililopo katika shule ya msingi ya Chalinze Modern Islamic iliyopo Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na kuathiri miundombinu ya bweni hilo ikiwemo vifaa vya kusomea na nguo za wanafunzi shuleni hapo 

Inaelezwa kuwa moto huo ulizuka wakati ambao wanafunzi walikua msikitini wakiswali swala ya alfajiri.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa kikosi cha zimamoto mkoa wa Pwani Jenifa Shirima amesema alipata taarifa za kuzuka kwa moto huo majira ya saa kumi na moja na dakika 42 alfajiri na kufika shuleni hapo ambapo walifanikiwa kuuzima moto huo kwa kushirikiana na uongozi wa shule watumishi pamoja na wanafunzi ambao hivi karibuni walipatiwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na majanga kama hayo.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Aboubakari Kunenge akizungumza mara baada ya kufika katika eneo la tukio amesema licha ya ajali hiyo kuteketekeza vibaya bweni la wavulana katika shule hiyo zikiwemo zana mbalimbali za kujisomea lakini hakuna mwanafunzi yeyote alidhurika kufuatia moto huo kwani wakati unazuka wanafunzi walikuwa msikitini wakiswali swala ya alfajiri.

Hili ni tukio la pili la ajali ya moto kuteketeza bweni ambapo mnamo mwezi Mei mwaka huu tulishudia bweni la sekondari ya wasichana Mkuza iliyopo Kibaha Pwani mali ya kanisa la KKKT likiteketea kwa moto wakati wanafunzi wakiwa katika ibada