Jumapili , 10th Aug , 2014

Mwanasiasa mkongwe na mjumbe wa halmashauri kuu ya chama tawala CCM Dkt Raphael Chegeni, ameungana na wanasiasa na wanaharakati mbalimbali kutaka Bunge Maalumu la Katiba lisitishwe.

Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa mbunge wa Busega Dkt Raphael Chegeni (kulia) akisalimiana na aliyewahi kuwa waziri mkuu Edward Lowassa.

Dkt Chegeni ambaye amewahi kuwa mbunge wa Busega kwa tiketi ya CCM, amesema mchakato wa katiba ni wa maridhiano na kuonya kuwa mvutano unaoendelea sasa baina ya wajumbe wa bunge maalumu la katiba hautowasaidia watanzania kupata katiba mpya.

Kwa mujibu wa Chegeni, bunge maalumu la katiba linaloendelea mjini Dodoma halitaweza kupata maridhiano pasipo kuwagawa Watanzania ambapo ameshauri bunge hilo kusimama kwanza kupisha chaguzi zijazo.

Wakati huo huo, vyuo vikuu vitano barani Afrika kikiwemo chuo kikuu cha Bagamoyo nchini Tanzania vimeunda mtandao wa pamoja utakaotoa mafunzo kwa wataalam wa serikalini ya namna ya kuingia mikataba kwa lengo la kulinda rasilimali za nchi husika zisiendelee kupotea kwa kisingizio cha uwekezaji.

Makamu mkuu wa Chuo kikuu cha Bagamoyo Dkt. Mtalo Elifuraha amesema baadhi ya watalaam wanaoingia mikataba na nchi zilizoendelea wamekosa uelewa wa namna gani mikataba hiyo itainufaisha nchi au kuipa nchi husika hasara.

Dk. Elifuraha amesema kuwa wanampango wa kuanzisha shahada za jinsi ya uingiaji mikataba katika vyuo hivyo ili kuweza kuwapa mwanga zaidi watu wanaoingia mikataba katika nchi za Afrika.