Jumatatu , 11th Sep , 2017

Ndani ya bunge la Tanzania leo mgogoro umeibuka  dhidi ya Wabunge wa CUF, upande wa Mwenyekiti  Prof Ibrahim Lipumba  na  wale wa Katibu Mkuu, Maalim Seif baada ya Mbunge wa Mtwara Mjini Maftaha Nachuma kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wao ndani ya Bunge.

Lipumba kushoto, Seif kulia

Mvutano huo ulianza baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson kutangaza kuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai amepokea barua kutoka kwa Kaimu Katibu wa CUF, Magdalena Sakaya kuhusu safu hiyo mpya ya uongozi.

Aidha baada ya tangazo hilo Mbunge wa Malindi, Ally Salehe aliomba mwongozo wa Spika wa kutaka kujua nani anaamua kuhusu uongozi wa wabunge bungeni kwa sababu wao wameshafanya uchaguzi wao na kumchagua Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea kuwa Mwenyekiti wao baada ya wabunge wanane wa chama hicho kuvuliwa uanachama hivyo kupelekea kupoteza sifa ya ubunge.

Pamoja na Muongozo huo Salehe amehoji kuwa inawezekanaje kuwepo na viongozi wawili bila uongozi wakwanza kufutwa.

Akijibu muongozo huo Naibu spika, Dk Tulia amesema Spika amepokea taarifa ya viongozi hao lakini hajapokea taarifa ya uchaguzi wa upande wa akina Salehe ambao unamuunga mkono Katibu Mkuu Maalim Seif.