Jumatatu , 1st Mar , 2021

Serikali imesema kuwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, itahakikisha inawafuatilia Watanzania wenye fedha wanaoishi nje ya nchi ili waweze kuja kuwekeza hapa nchini kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.

Waziri wa Ofisi ya Rais Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo

Kauli hiyo imetolewa leo Machi Mosi, 2021, na Waziri wa Ofisi ya Rais Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akizungumza kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio na kuwasisitiza Watanzania kufanya uwekezaji ndani ya nchi bila kusahau suala la ulipaji wa kodi.

"Kwenye sekta ya uwekezaji tunachokifanya kwa sasa moja ya mkakati wetu tunalenga watu, na mmoja wa mtu ambaye tumemlenga ni Diaspora, kuna Watanzania wengi wanaishi nje ya nchi wamekaa miaka 10 hadi 30 wanahela huko, kwanza tunaanza kuwatambua kupitia Wizara ya Mambo ya Nje Watanzania wanaoishi nje wenye visenti ili waje kuwekeza," amesema Prof. Mkumbo.

Akizungumzia suala la ulipaji wa kodi, Prof. Kitila, ameitaka Mamla ya Mapato nchini (TRA), kudai kodi kwa ustaarabu, "Ni lazima wenzetu wanaokusanya kodi watoe taarifa sahihi, lakini pia wajue kukusanya kodi ni 'customer care' siyo waende kipolisi, kwa hiyo watu wa TRA ifike mahala wajue kwamba Watanzania wengi ni wazuri waende kudai kodi wakijua huyu atalipa".