Jumatano , 13th Sep , 2017

Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo, kikisisitiza uchunguzi wa kushambuliwa Mbunge Tundu Lissu ufanywe na vyombo vya kimataifa familia yake  imezungumza kuhusiana na tukio hilo  na kusema wao hawana mashaka na jeshi la polisi kufanya uchunguzi.

Mbunge Tundu Lissu

Kauli hiyo ya familia imetolewa Jijini Arusha na Wakili Alute Mughwai ambaye ni kaka wa Tundu Lissu ambapo amesema mpaka sasa familia haijatoa maamuzi ya moja kwa moja ni nani achunguze tukio hilo lakini mpaka sasa wana imani na uchunguzi unaofanywa na jeshi la polisi.

Wakili Mughwai amesema pindi familia ikikaa kwa mara nyingine watazungumzia suala hilo na kuja na kauli nyingine ya pamoja ya familia kuhusiana na msimamo wao wa ni nani afanye uchunguzi wa tukio hilo kama kutakua na ulazima wa kufanya hivyo.

"Hatujakaa sisi kama wanafamilia kutoa msimamo wetu kuhusiana na uchunguzi wa tukio hilo, kwamba hatuna imani na jeshi la polisi na uchunguzi ufanywe na vyombo vya kimataifa lakini kama tukikutana tukawa na msimamo wetu tutatoa maoni yetu kama haja itakuwepo," amesema Mughwai.

Aidha ameongeza kwamba wao kama familia hawana tatizo lolote la kibiashara, wala hawana tatizo na Tundu Lissu hivyo watu wasije wakaunganisha matukio na kuhusisha kushambuliwa kwake na matukio ya biashara na kuongeza kuwa ndugu yao siyo mfanyabiashara bali biashara yake ni siasa pamoja sheria.

Mbali na hayo amewataka jeshi la polisi kuanzia uchunguzi wao kwa kufuatilia mkutano aliokuwa akizungumzia suala la Bombadier kukwama nchini Canada na alipozungumzia suala la kufuatiliwa na watu asiowafahamu.

Hata hivyo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema jana kilisema kinahitaji serikali iruhusu wachunguzi wa kimataifa kuingia nchini kufanya uchunguzi juu ya shambulio la kupigwa risasi kwa  Mbunge na Mwanasheria wao Tundu Lissu mnamo Septemba 7 mwaka huu mchana eneo la 'Area D' mjini Dodoma

Msikilize hapa chini Wakili Alute Mughwai

Sauti ya Kaka wa Lissu Alute Mughwai
Msikilize zaidi Kaka wa Lissu Wakili Mughwai