Ijumaa , 18th Sep , 2020

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, ameongezewa mwaka mmoja wa kuendelea  kuongoza Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki Mwa Afrika (EAPCCO).

IGP Simon Sirro

IGP Simon Sirro ameelezea uamuzi huo wa kubakishwa kwenye nafasi hiyo leo ambapo amesema hatua hiyo inakuja kutokana na kutokumalizia programu zake kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Corona.

"Huu ni mkutano wetu ulikuwa wa mwisho ambao toka mwaka jana mimi nilikuwa mwenyekiti wa EAPCCO kwa hizo nchi 14 jambo kubwa lilikuwa ni kuchagua mwenyekiti mwingine kwa mwaka mmoja tena, kwahiyo nitaendelea kuwa mwenyekiti wa EAPCCO", amesema IGP Sirro

Akifafanua juu ya uteuzi wake amesema, "Kutokana na ugonjwa wa Corona uliotokea naona wakuu wa jeshi la polisi ambao ni wanachama wa EAPCCO kila mtu alikuwa anasema program nyingi sijazimaliza lakini tulikuwa tunataka tuwakabidhi wenzetu wa DRC lakini na nchi hiyo nayo bado haijatulia kwahiyo wameshawishi nibaki kuwa mwenyekiti” amesema IGP Sirro.

Aidha amesema kuwa wameweka maadhimio kwa mwaka 2020/2021 katika kuwatafuta magaidi, kupeana taarifa na kupambana na makosa yanayovuka mipaka na kuhakikisha wanayashughulikia na wananchi wanaishi kwa amani.