Jumatatu , 29th Mei , 2017

Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Simon Sirro baada ya kuapishwa leo na Rais Magufuli amefunguka na kusema kazi yake ya kwanza kufanya ni kuhakikisha uhalifu unakwisha ili Watanzania waishi kwa amani nchini mwao.

ais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamishna wa Polisi Simon Sirro kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la polisi nchini Mei 29,2017 Ikulu jijini Dar es salaam

Simon Sirro amedai uhalifu nchini unaweza kupungua kama kutakuwa na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na jeshi la polisi nchini sababu wahalifu hao wanaishi katika jamii zetu hizi hizi. 

"Kipaumbele kikubwa ni uhalifu hivyo kazi yangu ni kuhakikisha uhalifu unapungua kwa kiasi kikubwa ili Watanzania waishi kwa amani lakini uhalifu huu utapungua tukipata ushirikiano mzuri na jamii, sababu hao wahalifu wanaishi kwenye jamii kwa hiyo ombi langu kwa Watanzania ili waishi kwa amani na utulivu ni vizuri sana watoe ushirikiano kwa jeshi la polisi. Naamini kabisa tutaweza sababu hawa wahalifu ni wachache kuliko sisi kwa hiyo umoja wetu ule lazima tutashinda" alisema Sirro 

IGP Simon Sirro

Mbali na hilo IGP Sirro ametoa onyo kwa wahalifu wote nchini akiwataka waache mara moja kwani mwisho wa siku watapoteza tu maisha yao na kuacha familia zao zikipata shida.

"Lakini niwape onyo wahalifu kuwa uhalifu haulipi, kung'ang'ania uhalifu mwisho wa siku utaacha familia yako hivyo ni afadhali ufanye kazi ya halali itakusaidia kulea familia yako lakini ukijiingiza kwenye uhalifu wa ujanja ujanja haitakusaidia kitu, mwisho utaacha familia yako" alisisitiza IGP Sirro