Jumatatu , 11th Sep , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amemuapisha Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu, ambaye alimteua kushika wadhifa huo Septemba 10, mwaka huu.

Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma akiwa Rais Magufuli.

Katika hafla hiyo ambayo imefanyika Ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa wakiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mh. Job Ndugai na Majaji wengine wa Tanzania, Jaji Ibrahim Juma amesema anashukuru kwa kurasimishwa kushika wadhifa huo ambao alikuwa ana ukaimu takriban miezi nane mpaka alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu.

Katika hotuba yake ya kwanza Jaji Mkuu Ibrahim Juma ameahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa weledi ikiwemo kulinda sheria na kuweka imani kwa wananchi, kwani wao ndiyo watetezi wao.

"Jambo ambalo ni muhimu kwetu sisi katika kufanya kazi ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwa na imani ya wananchi, kwa sababu wananchi wasipokuwa na imani na mahakama pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama hawatakuja kwetu ili kutatua matatizo yao", alisema Jaji Mkuu Ibrahim Juma.

Jaji Ibrahim ameendelea kusema kwamba "tumejiwekea mipango ya kuhakikisha tunaendelea kupata imani ya wananchi wetu, na tutafanya hivyo kwa kuepuka utovu wa maadili, vitendo vya rushwa na ucheleweshaji wa mashauri".

Ibrahim Juma alianza kutumikia wadhifa wa Kaimu Jaji Mkuu tokea Januari 18 mwaka 2017, baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu wa nchi Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kustaafu.