Jumatano , 21st Jun , 2017

Rais John Magufuli amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa Kiwango cha mita za ujazo za maji kwa matumizi ya mtu mmoja kitapungua hadi kufikia mita za ujazo 883 ifikapo mwaka 2035 kutokana na uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji.

Rais Magufuli amefunguka hayo leo katika siku ya pili ya ziara yake Mkoani Pwani ambapo akiwa katika eneo la Mlandizi wakati wa uzinduzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu, amezitaka mamlaka na wananchi kuchukua hatua stahiki katika kuendelea kulinda vyanzo vya maji.

Akizungumzia kuhusu deni la shilingi bil 40 ambazo taasisi mbalimbali za serikali zinadaiwa na idara ya maji  Rais Magufuli ametaka taasisi hizo zikatiwe maji mpaka pale zitakapolipa madeni yake.

“Mtu asipolipa bili ya maji iwe taasisi yoyote hata kama ni Ikulu narudia kusema KATA, kwa sababu tumezoea kudekezana” alisema Magufuli

Pamoja na hayo Rais amemshukuru Waziri Mkuu wa India kwa kutoa kiasi cha shilingi tril 1.3 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji katika mikoa 16 nchini pamoja na kumhakikishia Balozi wa India kuwa mahusiano kati ya nchi hizo yataendelea kuimarika.