Jumatano , 18th Oct , 2017

Kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Kenya, Bi. Roselyn Akombe, amejiuzulu nafsi yake kwenye tume hiyo, akisema uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 26 sio wa kuaminika, hivyo hataki kuwa sehemu ya uchaguzi huo.

Bi Akombe ametoa taarifa hiyo ikiwa zimebaki siku 7 tu uchaguzi ufanyike, akiwa nchini Marekani ambako alienda baada ya uchaguzi wa Oktoba 8, na kusema kuwa uchaguzi hautaweza kufikia matarajio ya wengi ya kuwa wa huru, haki na wenye kuaminika, huku akiilaumu Tume hiyo kuwa sehemu ya machafuko ya kisiasa yanayojitokeza nchini Kenya.

“Tunahitaji Tume ijiamini na kuzungumza kwamba uchaguzi huu hautaweza kufikia malengo ambayo utafanya uaminike. Si wakati wafanyakazi wanapata maelekezo ya dakika za mwisho juu ya mabadiliko katika teknolojia. Si wakati katika sehemu za nchi, mafunzo ya maafisa wa uongozi yanakimbizwa kwa hofu ya mashambulizi kutoka kwa waandamanaji" amesema.

Pamoja na hayo ameongeza kuwa "Uamuzi wangu wa kuondoka IEBC utawasikitisha baadhi yenu, lakini si kwa sababu nilikosa kujaribu. Nilijaribu kadiri ya uwezo wangu ukizingatia hali na mazingira yaliyopo. Wakati mwingine, unalazimika kusalimu amri na kuondoka, hasa wakati maisha ya watu yamo hatarini," amesema kwenye taarifa hiyo".

Aidha Bi Akombe amesema kwamba  imekuwa vigumu kuendelea na mikutano ya tume ambapo Makamishna kila wakati wanalazimika kupiga kura kufanya maamuzi kwa kufuata msimamo wao badala ya kuangazia uzito wa jambo linalojadiliwa. ikiwa ni pamoja na kushindwa kutokea kwenye televisheni kutetea misimamo ambayo anatofautiana nayo kwa sababu ya kuwajibika kwa pamoja.

Mbali na hayo Bi. Akombe amesema amefikia uamuzi kwamba hawezi tena kutoa mchango wa maana kwa Tume na kwa taifa lake kama Kamishna.

Dkt Akombe alizuru Nyanza na maeneo ya Magharibi, ambayo ni ngome ya upinzani, wiki iliopita huku tume hiyo ikijaribu kuwafunza maafisa watakaosimamia uchaguzi huo.