Jumanne , 15th Sep , 2020

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeutaka upande wa mashtaka kufuatilia jalada la kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo na mwenzake ambalo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).

Archard Kalugendo

Mbali na Kalugendo mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mthamini Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu ambao wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh Bilioni 2.4.

Wakili wa Serikali, Faraja Ngukah amedai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo kwa DPP kusubiri maelekezo hivyo, aliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko amedai kesi hiyo ni ya tangu 2017 na kwamba taarifa hiyo kuhusu jalada kuwepo kwa DPP ni ya muda mrefu, hivyo kama inawezekana apelekwe muhusika kwa DPP ili aeleze ni lini maelekezo hayo yatatoka kusudi wateja wake wapate nafuu.

Akijibu hoja hiyo, Ngukah amesema wanatambua kuwa jalada hilo ni la muda mrefu na wanalifanyia kazi ambapo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 29, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kuelekeza upande wa mashtaka kufuatilia jalada hilo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh  2,486,397,982.54, ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017  katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Shinyanga.