Jumanne , 19th Sep , 2017

Mtoto mchanga mwenye siku tano tangu azaliwe ameokotwa na wapita njia katika mji wa East London nchini Afrika Kusini, akiwa kwenye mfuko wa takataka huku akiwa amevirigwa na tshirt, na ujumbe mzito kwa atakayemuokota.

Msemaji wa Polisi wa eneo hilo Nkosikho Mzuku amesema mtoto huyo ambaye ni wa kiume alipatikana siku ya Jumamosi baada ya watoto waliokuwa wakipita kwenda kwa mwalimu wao, na kukuta mfuko huo.

Kwenye mfuko huo walikuta kikaratasi chenye ujumbe ambao unaaminika kuwekwa na mama yake, akiomba kwa yeyote atakayemuokota mtoto huyo ampeleke sehemu salama.

“Tafadhali mchukue mtoto huyu na mpeleke kituo cha polisi, baba yake anataka kumuuza, nimekimbia naye lakini najua atatutafuta, ni bora nife mimi kuliko mtoto kwa sababu hana hatia, nimejifungua mtoto huyu Septemba 14, 2017, ahsanteni na Mungu akubariki”, ulisomeka ujumbe huo ambao ulikutwa kwa mtoto huyo.

Jeshi la polisi nchini Afrika Kusini limesema linaendelea kumtafuta mama wa mtoto huyo na kumtia mikononi mwa sheria.