Jumanne , 17th Oct , 2017

Waziri wa Maliasili ya Utali Dkt. Hamis Kigwangala amesema kuwa ugeni wa Serikali ya Oman nchini kwa Wizara hiyo utatoa fursa ya kujifunza kwa kuangalia Serikali hiyo inafanya nini ili kuweza kuimarisha Sekta ya Utalii nchini.

Mh. Kigwangalla amesema hayo leo wakati Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu leo alipokutana na ujumbe wa Mfalme wa Oman Sheikh Sultan Qabous Bin Said ambao unadaiwa kuwa na malengo ya kuimarisha masuala ya biashara kwa nchi za ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki. 

“Tumekuja kuangalia na kujifunza wenzetu wanafanyaje katika mbinu za sekta ya utalii kwa mfano serikali ya Oman ina tembelewa na watalii zaidi ya milioni 3.2 kwa mwaka lakini kwa Tanzania sisi tunatembelewa na watalii milioni 1.2, kwa hiyo ugeni huu utaimarisha ushirikiano wa pamoja na Oman katika sekta hii”, alisema Dkt. Kigwangala

Aidha Dkt. Kigwangala alisema wataanzisha ushirikiano wa mradi wa watalii kuja moja kwa moja kutoka Oman mpaka Tanzania na Pwani ya nchi za Afrika Mashariki.

Naye Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa ujio wa ugeni huo kutoka Oman ni fursa nzuri ya kufanya utafiti wa maeneo ya mafuta kwani serikali ya Oman ni wazoefu na wajuzi katika masuala ya uchimbaji mafuta.

“Tunatarajia ujio huu utajenga uhusiano mzuri katika hatua za utafiti wa mafuta hapa nchini ili kuweza kujenga uzoefu kwa watafiti wetu na kuwawezesha watanzania kuchimba mafuta bila shida kwa sababu wenzetu ni wazoefu katika eneo hili la
kiuchumi”
, amesema Dkt. Kalemani.