Jumanne , 1st Dec , 2020

Baada ya kukaa miaka 20 bila kuwa na shule ya msingi, wananchi wa Kijiji cha Lelgu wilayani Kiteto mkoani Manyara hatimaye wamefanikiwa kujenga madarasa saba na kufanikiwa kukamilisha manne na kuiomba serikali kuwasaidia katika kupaua madarasa yaliyobaki.

Miongoni mwa majengo ya shule yaliyojengwa na wananchi wa Kijiji cha Lelgu.

Mbali na hilo wananchi hao pia wameiomba serikali kuipatia shule hiyo usajili ili kuondoa adha ambayo walikuwa wakiipata watoto wao, kutembea umbali mrefu na wakati mwingine kukosa masomo

Wakizungumza na EATV wananchi hao akiwemo Kipongo Sabulei na Ester Lemati, wamesema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na wananchi katika kujitolea kwa hali na mali ili kufanikisha kijiji chao kuwa na shule jambo ambalo kwa sasa wamekamilisha madarasa hayo.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kiteto, Edward Ole Lekaita, amepongeza jitihada hizo za wananchi na kusema hatokuwa nyuma katika kuwasaidia wananchi ambao wamekuwa wakielekeza nguvu kubwa katika kuibua miradi wao wenyewe.