Jumapili , 26th Feb , 2017

Mbunge wa Chalinze mkoani Pwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwan Kikwete, amesema anaitamani nafasi aliyonayo Abdulrahaman Kinana ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa.

 

Kikwete alizungumza hayo baada ya kuulizwa swali kama ana ndoto ya kugombea nafasi ya urais, ambapo alikataa huku akisema anaitaka nafasi ya Kinana ndani ya chama hicho.

“Sijawahi kutamani kuwa Rais ila muda ukifika natamani kuwa Katibu Mkuu wa CCM”. Alisema Kikwete katika mahojiano na moja ya chombo cha habari Jijini Dar es Salaam.

Aidha Mbunge huyo alisema mafanikio yote aliyonayo ni kutokana na malezi bora aliyopatiwa kutoka kwa baba yake aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

“Malezi yangu kuzaliwa na kiongozi kumenisaidia kufikia hapa, nisingezaliwa huko labda ningekuwa mtu tofauti na nilivyo, mzee wangu ana mchango mkubwa hata jimboni ananipa changamoto, ananielekeza pamoja na kunishauri”. Alisema Kikwete