Jumatano , 22nd Nov , 2017

Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dkt. Jakaya Kikwete amekubali shamba lake la mifugo lililopo kijijini kwake Msoga Bagamoyo litumike kama shamba darasa.

Mh. Jakaya Kikwete amekubali ombi hilo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo mkoani Morogoro, baada ya kutembelea chuoni hapo akiwa na wataalamu wake wa mifugo kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali kuhusu kilimo na mifugo.

Uongozi wa SUA ukatumia nfasi hiyo kuwasilisha ombi lao kwa Mh. Kikwete ambaye alikubali na rasmi kuingia makubaliano ya pamoja ili kulitumia shamba lake la mifugo kama shamba darasa la kutolea elimu ya vitendo kwa wanafunzi wao, wataalamu wa mifugo na wafugaji.

Aidha Rais Mstaafu ameeleza kulizishwa na mafunzo aliyoyapata chuoni hapo na kutoa ahadi ya kuendelea kushirikiana na chuo hicho kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kisayansi ya sekta ya ufugaji iweze kumletea tija mfugaji.

Rais Mstaafu Kikwete kwa sasa amejikita zaidi kwenye suala la ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, kilimo cha mazao ya chakula na matunda hasa mananasi kijijini Msoga, Chalinze , wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani.