Alhamisi , 8th Dec , 2016

Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imesema itaanza kuwapima wananchi kupitia makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi kubaini endapo wanatumia dawa za kulevya ili hatua stahiki zichukuliwe.

Prof Samuel Manyele - Mkemia Mkuu wa Serikali akiwa na ya Studio za EA Radio

Ofisi hiyo itakuwa ikiangalia sumu ambazo hupatikana kutokana na matumizi ya dawa ya kulevya, zoezi ambalo litafanyika kwenye mashule, madereva na sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi lengo likiwa ni kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.

Hayo yamesemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samweli Manyele wakati akizungumza na EATV na East Africa Radio kuhusu jitihada zinazochukuliwa na serikali katika kudhibiti sumu ambazo zinauzwa mitaani bila kuwa na maelezo elekezi ya kuzitumia na kusababisha madhara kwenye jamii inazozitumia.

Amesema kuwa zoezi hilo la upimaji sumu zinazopatikana kutokana na matumizi ya dawa za kulevya linafanyika baada ya serikali kufanikisha kuanzishwa kwa kitengo maalumu cha kuratibu matokeo ya sumu nchini ambacho kipo chini ya mkemia mkuu wa serikali.