Alhamisi , 25th Aug , 2016

Serikali imeahidi kusimamia kwa nguvu zote shilingi bilioni 33 zilizotengwa kwa ajili ya kukarabati shule kongwe kwa mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 ili kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Baadhi ya majengo katika shule ya Sekondari Mzumbe kama yalivyokuwa mwaka 2014

Pia imeahidi kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafukuza kazi wakurugenzi na wakuu wa shule watakaohusika na ubadhirifu wa fedha hizo.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, SULEIMAN JAFO ametoa ahadi hiyo leo mjini Dodoma katika kikao cha kamati ya utawala na serikali za mitaa kwa ajili ya kufanya tathimini ya mkakati wa serikali katika kutatua kero ya ukosefu wa madawati na miundombinu mingine katika sekta ya elimu.

Jafo amesema fedha hizo zimetengwa na serikali kwa ajili ya kukarabati shule kongwe 33 ambapo kila shule imetengewa shilingi bilioni moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa usimamizi wa elimu ofisi ya Rais TAMISEMI, Juma Kaponda, ametaja mikakati mingine ya serikali iliyopo kuwa ni ujenzi wa nyumba za walimu, maabara, matundu ya vyoo na madawati.

Kamati hiyo kesho itakutana na watendaji wa ofisi ya rais utumishi na utawala bora kwa ajili ya kujadili taarifa ya tathmini ya mkakati wa serikali wa kuondoa tatizo la watumishi hewa na mpango wa serikali kuhusiana na uboreshaji wa utumishi wa umma kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.