Ijumaa , 9th Apr , 2021

Waziri wa Madini Doto Biteko amesema Kiswahili kimekubalika kuwa moja ya Lugha ya Mawasiliano zitakazotumika katika Umoja wa nchi zinazozalisha madini ya Almasi Afrika.

Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na Wanahabari wakati akifunga Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) uliofanyika kwa Njia ya Video tarehe 8 Aprili, 2021 Jijini Dodoma.

Waziri Biteko amesema hayo wakati akifunga Mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika ( African Diamond Producers Association- ADPA) uliofanyika kwa njia ya Video Conference ambapo amesema Kiswahili kinaongezeka kwenye lugha zilizokuwa zinatumika awali ambazo ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.

Mkutano huo wa 7 wa Mawaziri wa Nchi zinazozalisha madini ya Almasi Afrika, umehudhuriwa na nchi zote 19 wanachama wa umoja huo.

Baadhi ya Nchi hizo ni Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea na Sierra Leone, Algeria, Jamhuri ya Congo, Cote D’ivore, Gabon, Liberia, Mali na Mauritania.