Jumanne , 17th Jan , 2017

Serikali imepanga kukomesha urasimu katika upatikanaji wa taarifa za serikali unaofanywa na baadhi ya maafisa habari wa umma, unaochangia ugumu katika utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya habari.

Waziri Nape Nnauye akisikiliza maelezo kutoka kwa mratibu wa vipindi wa EATV, Sophie Proches, wakati wa ziara ya ke katika studio za EATV Ltd.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amesema serikali kwa sasa inafanya mabadiliko makubwa ili kuhakikisha maafisa habari wote wanaufahamu wa mambo yaliyopo kwenye taasisi zao na kuweza kutoa taarifa kwa umma kwa wakati.

Ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam,alipotembelea  vyombo vya habari vya East Africa Television (EATV), ITV pamoja na Capital TV ziara ambayo aliambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk. Hassan Abbas pamoja na Mkurugenzi wa Utangazaji (TCRA) Fred Ntobi.

Waziri Nape pia amesema serikali ina mpango wa kuboresha sheria na kanuni mbalimbali ambazo ni kikwazo katika tasnia ya habari nchini, kwa kuwa yeye ndiye mwenye dhamana ya kupeleka mabadiliko ya sheria bungeni.

Waziri Nnauye amevipongeza vyombo vya habari vya IPP kwa kazi nzuri inayofanya na kuvitaka kushiriki kikamilifu katika kuchangia kusaidia kufanikisha utekelezaji azma ya serikali ya awamu ya tano, ya Tanzania ya viwanda na mapinduzi ya kilimo.

Mhe. Nnape amesema kuwa lengo la ziara yake hiyo ni kukutana na wadau wa habari kutaka kujua changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na kuangalia mambo yanayowakwanza katika Sheria na Kanuni zilizopo ili zibadilishwe na kusaidia kukua kwa sekta ya habari nchini.