Jumamosi , 24th Sep , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk Beatrice Byalugaba kufanya uchunguzi na kubaini madaktari wa hospitali ya wilaya ya Mafia wanaomiliki maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo na kuwachukulia hatua.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk Beatrice Byalugaba kufanya uchunguzi na kubaini madaktari wa hospitali ya wilaya ya Mafia wanaomiliki maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo na kuwachukulia hatua.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo alipotembelea hospitali ya wilaya ya Mafia katika siku ya pili ya ziara yake wilayani humo, ambapo amesema ameshangazwa kukuta maduka ya dawa yanayomilikiwa na madaktari nje ya hospitali hiyo, kwani tayari serikali ilishaagiza kuondolewa kwa maduka ya madaktari karibu na hospitali wanazofanyia kazi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupatiwa matibabu bure kwa kipindi cha mwaka mzima.

Awali Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Joseph Mziba alisema mwamko wa wananchi kujiunga na mfuko wa CHF ni mdogo jambo linalokwamisha upatikanaji wa huduma za afya wilayani Mafia. Jumla ya wananchi waliojiunga na CHF ni watu 6,000 kati ya watu 50,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Eric Mapunda ameiomba Serikali kutoa kibali kwa halmashauri kununua dawa ambazo zinakosekana MSD kwenye soko moja kwa moja bila ya kupitia utaratibu wa manunuzi.

"Kuna wakati tunakosa dawa MSD na kulazimika kununua kwa mawakala kwa kufuata taratibu ya manunuzi. Tunalazimika kununua boksi moja ambapo boksi moja la panadol linauzwa sh. 20,000 na tukinunua moja kwa moja sokoni bila ya kufuata utaratibu huo boksi hilo hilo tunalipata kwa sh. 8,000,”alisema