Jumamosi , 23rd Jul , 2016

Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amechaguliwa leo (Julai 23, 2016) Dkt John Pombe Magufuli, leo ametangaza kufanya mageuzi makubwa ndani ya chama hicho chini ya uongozi wake.

Dkt John Pombe Magufuli,

Akitoa hotuba yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwa kupata asilimia 100 ya kura za NDIYO za wajumbe 2,398, Magufuli ameweka hadharani dira yake ndani ya chama inayotoa mwelekeo kwa kutumia mikakati minne ili kukiboresha na kukiimarisha chama hicho.

Jambo la kwanza atakalolifanya ni kuimarisha utendaji wa chama ili kujenga chama madhubuti kitakachoweza kuisimamia serikali. Katika hilo amesema kuwa atapitia upya baadhi ya nafasi za uongozi ndani ya chama na kuondoa vyeo ambavyo havina tija.

Katika hilo amesema atahakikisha nafasi zinazobaki ni zile zinazoendana na wakati uliopo, huku akionesha kushangazw na uwepo wa nafasi za chipukizi, ukamanda wa vijana, ushauri wa Jumuiya ya Wazazi n.k

“Hivi kuna umuhimu gani wa kuwa na chipukizi mwenye umri wa miaka 8 hadi 10 katika kipindi hiki badala ya kumuacha mtoto huyo asome? Sisi tukiwa na chipukizi, je Chadema wakiwa na chipukizi, je CUF wakiwa na Chipukizi hawa watoto watasoma saa ngapi” Amehoji Dkt Magufuli.

Pia ameahidi kufuatilia mali zote za chama na kuhimiza wanachama kulipa ada zao za uanachama kielektroniki, huku akisisitiza wanachama kuwajibika kucha kazi, huku akiahidi kuwapa nafasi vijana wenye uwezo na elimu stahiki badala ya mtu mmoja kuwa na idadi kubwa ya vyeo.

Jambo la pili ni kuongeza idadi ya wanachama huku akisisitiza kuwa siasa ni mchezo wa namba hivyo amejipanga kuvuta wanachama wengi hususani vijana. Amesema mpango huo utafanikiwa kwa kuhakikisha CCM inatekeleza ahadi zake.

Jambo la tatu alilopanga kushughulikia ni mapambano dhidi ya rushwa huku akikiri kuwa ndani ya CCM kuna rushwa kwa kiasi kikubwa, hivyo ameahidi kuwachukulia hatua wote watakaobainika kujihusisha na rushwa ndani ya chama kinyume na sheria za nchi na kanuni za chama.

“Bahati mbaya hata chama chetu CCM ni miongoni mwa taasisi ambazo zina tatizo kubwa la rushwa, lazima niseme ukweli, .. Rushwa ndiyo imekuwa kigezo cha mtu kupata uongozi, nimedhamiria kushirikiana nanyi kuondoa rushwa.. Katika uongozi wangu, mtu atakayetumia rushwa hatachaguliwa au hatateuliwa kugombea nafasi yoyote” Ameeleza rais Magufuli.

Jambo la nne alilopanga kulifanya ni kuondoa wasaliti ndani ya chama. Amesema ndani ya CCM kuna watu wengi ambao mchana wanakuwa CCM lakini usiku wanakuwa wanaunga mkono upinzani.

“Ni bora kuishi na mchawi kuliko kukaa na msaliti, hatutaki CCM pandikizi, hatuhitaji wana CCM ambao wapo kwa kuwa wanamuabudu mtu fulani, tunahitahitaji wana CCM ambao usiku, mchana, mvua ikinyesha, jua likiwaka wanabaki CCM tu, Nataka CCM iwe ya wanyonge” Amesisitiza.

Pia Magufuli ambaye pia ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametumia nafasi hiyo kuelezea mambo ambayo serikali ya awamu ya tano imeyafanya kwa kipindi cha miezi 8 tangu kuingia madarakani mwezi Novemba mwaka jana.

Amesema katika kipindi hiki kifupi serikali imeweza kutoa elimu bila malipo kwa kutenga shilingi bilioni 18 kila mwezi, imenunua ndege mbili mpya ambazo zitaingia nchini mwezi Septemba, imetangaza tenda ya ujenzi wa reli ya kati, imesaini makubaliano ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga, imeweza kuimarisha nidhamu ya utumishi wa umma na kuondoa wafanyakazi hewa zaidi ya 12,500 pia imeweza kudhibiti matumizi ya fedha za umma na kuongeza kiwango cha makusanyo ambapo kwa sasa serikali inakuanya wastani wa trillion shilingi 1.2 kila mwezi.

Mkutano huo mkuu maalum umehudhuriwa na wajumbe 2,398 sawa na asilimia 99.4 ya wajumbe wote 2,412 kutoka nchi nzima, pamoja na waalikwa mbalimbali vikiwemo vyama 12 vya siasa ambavyo ni Chaumma, UDP, TLP, ADC, UMD, Jahazi Asilia, Chausta, UPDP, AFP, DP, CCK, SAU.

Waalikwa wengine ni mabalozi 39 wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.