Jumatatu , 18th Sep , 2017

 Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi aliyekuwa Naibu Waziri na Mbunge Mstaafu wa Mpwapwa  Bw Gregory Teu kufuatia vifo vya watu 13 ambao ni ndugu wa familia yake waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea  Uganda

Watu hao wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana na lori jana tarehe 17 Septemba, 2017 majira ya saa 4:00 Usiku katika barabara ya Masaka nchini Uganda wakiwa njiani kurejea Tanzania.

“Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa ya watu, nampa pole Ndg. Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa, nawapa pole wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi.

“Nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote wanaopata matibabu huko nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amewataka wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea.