Jumanne , 19th Sep , 2017

Waziri mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka  vijana kutumia fursa ya ajira ya viwanda kufanya kazi badala ya kuipoteza na  kuwaachia wawekezaji kuleta vijana kutoka nje.

Majaliwa alisema hayo leo alipotembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni kilichoko Kibaha na kiwanda cha kutengeneza vigae kilichoko Pingo halmashauri ya  Chalinze.

Amesema vijana wanatakiwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kufanya kazi ili waweze kupata ajira kwani katika viwanda ajira zinapatikana kwa watu wenye uwezo tofauti, wasomi na wasio wasomi.

Majaliwa pia amewagiza viongozi wa Halmashauri ya Kibaha na Chalinze  kuhakikisha wanatengeneza miundombinu yote ya barabara pamoja na kutenga maeneo ya viwanda  ili kuwavutia wawekezaji.

Mh. Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inasaidia kutatua changamoto  zinazojitokeza ikiwemo ukosefu wa maji katika mji wa Chalinze pia kuwezesha jeshi la zima moto kuwa na vituo vya kutosha vya kuzimia moto , sambamba na vitendea kazi ili kulinda maisha ya watu na mali pindi moto unapoweza kutokea.