Jumanne , 21st Nov , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli amepewa shukrani na pongezi kutoka Chama Cha Mapinduzi mkoani Mbeya.

CCM Mbeya imempongeza mwenyekiti wa chama hicho taifa Mh. John Pombe Magufuli kwa kumteua Mh. Mary Mwanjelwa kuhudumu katika nafasi kama Naibu Waziri wa Kilimo kwenye serikali ya awamu ya tano.

Pongezi hizo pamoja na shukrani zimetolewa na katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya Ndg. Wilson Nkambaku kwa niaba ya wajumbe wa kamati ya siasa wakati akitoa taarifa ya chama hicho ofisini kwake mara baada ya Naibu Waziri kuzuru katika ofisi hizo akiwa ziarani Mkoani Mbeya.

Katibu huyo amesema Rais Magufuli amefanya uteuzi muhimu kwani Mh. Mwanjelwa ni mchapakazi na msaada mkubwa kwa chama hicho, hivyo uteuzi huo umeonyesha imani kwa Chama Cha Mapinduzi na wananchi wa mkoa mzima wa Mbeya.

Aidha Nkambaku  amemsihi Naibu Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) mkoani Mbeya, kufanya kazi kwa bidii huku CCM ikiahidi kutoa ushirikiano mwema kwake.