Jumatatu , 30th Nov , 2020

Tatizo la uwepo wa fikra potofu kwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera kuwa wanaokula mboga za majani ni maskini, limetajwa kuchangia uwepo wa idadi kubwa ya watoto waliodumaa.

Pichani:Mfano wa mboga za majani

Akizungumza na EATV, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Desdery Karugaba amesema kuwa wanaendelea kuhamasisha wananchi wa mkoa wa Kagera kuachana na fikra hizo na badala yake kutumia mboga hizo kwa wingi hususani akina mama wajawazito.

“Mboga za majani zinahusishwa na umasikini lakini mtu anaona kuzitumia hizi mboga atakuwa ni kama mtu wa hali ya chini, sisi tunahamasisha matumizi ya hizi mboga kwa wajawazito si mboga tu anatakiwa ale mlo kamili kutoka yale makundi matano ya chakula, kila kundi lina kazi yake moja likikosekana lazima litatokea tatizo mwilini” amesema Desdery

Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Elieth Rumanyika, amesema tatizo la udumavu kwa watoto nchini linaendelea kushuka na sasa ni asilimia 31.8 huku wakizidi kuongeza nguvu katika kuhakikisha udumavu nchini kwa watoto chini ya miaka mitano unapungua na tatizo la wanawake ambao wana upungufu wa damu wanapungua.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na taasisi ya chakula na lishe Tanzania, mkoa wa Kagera una watoto 260,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano waliodumaa.