Jumamosi , 18th Nov , 2017

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi ameagiza kukaguliwa kwa mapato na matumizi ndani ya Kata ya Mgusu iliyopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani humo.

Mhandisi Luhumbi ametoa agizo hizo kwa  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita Mhandisi Modest Apolinary akimtaka apeleka wakaguzi wa ndani wa Hesabu za Serikali kwenye kata hiyo ya Mgusu ili wakakague na kujiridhisha.

“Mkurugenzi leta timu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ili ikague na kujiridhisha kama kuna fedha yoyote iliyochukuliwa
pasipo maelezo yanayojitosheleza hatua zichukuliwe haraka kwa wote watakaobainika kuhusika”, amesema Luhumbi.

Mkuu huyo wa mkoa yupo kwenye ziara yake mjini Geita akizindua kampeni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na Zahanati ambapo amepokea malalamiko ya wakazi wa Machinjioni katika kata ya Mgusu waliodai kutosomewa taarifa za mapato na matumizi ya fedha zao. 

Mheshimiwa Robert ameongeza kuwa ukaguzi huo ufanyike kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 kisha apate taarifa hiyo ofisini. Kwa upande mwingine Mhandisi Luhumbi amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na wananchi katika kujiletea maendeleo sambamba na huduma za jamii.