Alhamisi , 17th Dec , 2015

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mh. Charlses Kitwanga amewaagiza maofisa waandamizi wa jeshi la polisi kumpelekea maelezo hii leo kuwa wamejipangaje na watafanya nini katika kupambana na kuwamata wahusika wa dawa za kulevya.

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi,Mh. Charlses Kitwanga.

Mh. Kitwanga ametoa agizo hilo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jeshi la polisi kikiwemo chuo cha taaluma ya polisi, nyumba za polisi kurasini na kituo kikuu cha polisi jijini Dar es salaam.

Amesema tatizo la dawa za kulevya limekuwa kubwa hivyo ni lazima jeshi hilo kuhakikisha linakuwa na mpango wa kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na hatua zinachukuliwa bila kuangalia muhusika ana nguvu gani katika jamii au siasa.

Waziri huyo ameongeza kuwa endapo jeshi hilo litashindwa kuwakamata watu hao inaonesha kuwa wanashirikiana na wahusika hivyo ni lazima wakuhusika wakamatwe ili kuondoa dhana ya wao kushirikiana na watu hao.

Katika hatua nyingine amewataka kujipanga na kuondoa dhana iliyojengeka kwa watu kuwa askari wamekuwa wakiwabambikia watu kesi ambazo hawahusiki nazo na kuwataka kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa nidhamu na weledi.