Alhamisi , 15th Sep , 2016

Kukosekana kwa fedha ya kukamilisha mchakato wa sheria ya Parole kwa wafungwa mbalimbali nchini waliomaliza nusu ya kifungo chao gerezani ni miongoni mwa sababu yakuwepo mrundakano wa wafungwa katika magereza Tanzania.

Dkt Augustino Mrema

Akiongea na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaam wakati akimpongeza na kisha kumteua Mchungaji Dkt. Getrude Lwakatare kuwa mratibu wa harambee ya kuchangisha fedha kwaajili ya kuwalipia wafungwa wanaotakiwa kutoka gerezani chini ya sheria ya Parole Mwenyekiti wa bodi ya Parole Taifa Augustino Lyatonga Mrema amesema ili mfungwa atolewe gerezani ni lazima maofisa wa parole wafuatilie nakala ya hukumu.

“Ni lazima maofisa wa parole wafuatilie nakala ya hukumu kwenye mahakama iliyomukuhumu na waende kuonana na uongozi wa kijiji au mtaa ambapo mfungwa atenda kuishi anapotoka gerezani ikiwa ni pamoja na kuonana na familia yake na pia kuonana na watu waliowakosea ili jamii ya eneo hilo itambue kuwa ataachiwa huru” amesema

Aidha, Mrema amewataka maofisa wa parole kote nchini kuwatembelea wafungwa waliopata Parole ili wafungwa wengi wenye sifa za kutolewa kwa sheria ya Parole wasiendelee kuteseka magerezani bali waende kuungana na familia zao sambamba na kuongeza nguvu kazi.

Kutokana na kutotengwa fedha kwaajili ya kushugulikia suala hilo, Mwenyekiti huyo wa Parole Taifa, amemteua Mama Getrude Lwakatare kuwa mratibu wa kuchangisha fedha kwa kushirikisha viongozi wote wa dini nchini kushiriki harambee kwaajili ya kuchangisha fedha za kuwatoa wafungwa magerezani na kupunguza msongamano katika magereza nchini.

“Napendekeza kufanyike harambee kwenye makanisa yote nchini, siku ya Jumapili moja ili sadaka zote zikatumike kuwalipia faini wafungwa waliopo magerezani” amesema

Mrema amesisitiza kuwa wanaolengwa na Parole siyo wanye makosa ya ubakaji, mauaji, wizi kwa kutumia silaha na makosa mengine.

Naye Mchungaji Dkt. Getrude Lwakatare amewataka watanzania kuangalia taifa kwanza kwani kina baba wengi wenye nguvu watarudi katika jamii na kusaidia katika uzalishaji mali sambamba na kutatua matatizo ya kiuchumi na kimaendeleo katika familia zao.

“Tutaunganisha familia zilizo sambaratika na kutaabika baada ya mzazi mmoja kufungwa miaka 6 pengine kwa kukosa faini ya milioni moja tuu, tutaondoa msongamano wa wafungwa na kulinda afya zao kutokana na magonjwa wanayopata wakiwa gerezani” amesema

Mchungaji Gutrude Lwakatare amesema anaunga mkono jitihada za bodi ya Parole Taifa na siyo kuwalinda waalifu kama ambavyo wengine watatafsiri kwani kurejesha familia ni miongoni mwa kustawisha jamii huku akinukuu maneno ya kidini yanayolenga kuwakomboa walioko kwenye vifungo na taabu mbalimbali ndani ya jamii.

Dkt. Getrude Lwakater