Jumanne , 25th Jul , 2017

Jeshi la polisi mkoani Mwanza, linamshikilia mtu mmoja (39) kwa tuhuma za kumbaka mtoto (11) jana Jumatatu alfajiri katika mtaa wa  Wa Kabangaja Wilaya Ya Ilemela  na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri kitendo ambacho ni  kosa la jinai.

Kamanda Wa Polisi (M) Mwanza, DCP: Ahmed Msangi amesema kwamba tukio hilo limetokea asubuhi wakati wazazi wa majeruhi (jina limehifadhiwa)  wakiwa wametoka kwenda kutafuta riziki na hapo ndipo mtuhumiwa ,( Makusudi Rashid) alipopata nafasi ya kufanya uhalifu huo

"Majira tajwa hapo juu wazazi wa majeruhi aliyebakwa waliondoka na kwenda kutafuta riziki ya watoto huku nyumbani wakiwaacha majeruhi na mdogo wake wakiwa wamelala. inasemekana kuwa wakati majeruhi akiwa amelala na mdogo wake, ghafla alishtuka na kumuona mtuhumiwa tajwa hapo juu akiwa anambaka kwa nguvu huku akisikia maumivu makali na kupelekea kupiga kelele za yowe akiomba msaada,"  Kamanda Msangi alieleza.

Ameongeza kuwa baada ya majeruhi kuomba msaada mtuhumiwa alikimba "Wananchi walimuona mtuhumiwa  akiwa anakimbia na kuanza kukimbiza hadi walipofanikiwa kumkamata kisha wakatoa taarifa kituo cha polisi, askari walifanya ufuatiliaji wa haraka juu ya taarifa hizo hadi eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi wa wananchi". 

Hata hivyo Kamanda msangi amesema kwamba polisi wapo kwenye mahojiano na mtuhumiwa, pindi uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani, huku majeruhi akiwa tayari amepelekwa hospitali kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Vilevile Kamanda msangi amewataka wazazi pamoja na walezi kuhakikisha wanawawekea watoto makazi salama yatakayoweza kuwalinda watoto na mali dhidi ya wahalifu pia anawataka wananchi wa mwanza kuwa waangalifu na makini wakati wote na watu wenye nia ovu dhidi ya watoto.