Jumanne , 21st Nov , 2017

Mwanasheria maarufu nchini Alberto Msando ambaye amewahi kuwa mwanachama wa Chadema pamoja na ACT-Wazalendo amehamia Chama cha Mapinduzi.

Msando ameomba ridhaa ya kujiunga na CCM leo kwenye mkutano mkuu wa Halmashauri kuu ya NEC unaoendelea jijini Ikulu Dar es salaam na kukubaliwa na wanachama chini ya mwenyekiti wa chama hicho Rais John Pombe Magufuli.

“Nimeona harakati nyingi za serikali na Chama cha Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo wananchi hivyo nimekaa nakajitathimini nimeamua kujiunga na CCM ili nisaidie kusukuma gururudumu la maendeleo.

Msando pia ameeleza kuwa alikuwa anaona anachelewa kujiunga na vijana wenzake kama Mbunge wa Dodoma Mjini Antony Mavunde ambao mara zote amekuwa akiwaona wapo mstari wa mbele katika kupigania maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla.

Aidha Msando ambaye amewahi kuwa mshauri wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema hii ni mara yake ya kwanza kuingia CCM kwa kuwa kwa sasa si aibu tena kwa mtu kujitambulisha kuwa ni mwana CCM kwani imesafishika kuliko ilivyokuwa awali ambapo ulikuwa ukionekana na nguo za CCM unazomewa mitaani.