Alhamisi , 23rd Mar , 2017

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye amewaaga rasmi wanahabari nchini baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo leo, huyu akiwaachia ujumbe wa kuwataka wasiwe waoga.

Waziri Nape akizungumza na wanahabari akiwa juu ya gari

Nape aliyezungumza na wanahabari nje ya hotel ya Protea Jijini Dar es Salaam katika mazingira magumu baada ya kuzuiwa na polisi kufanya hivyo, amewashukuru wanahabari kwa ushirikiano wao kwa muda wa mwaka mmoja aliokaa kwenye wizara hiyo.

"Niko hapa kuwashukuru wanahabari kwa ushirikiano mlionipa kwa mwaka mmoja, nimewapenda sana sana sana...nilisema kuna gharama ya kulipa katika kusimamia haki za watu, na mimi niko tayari kulipa gharama hiyo..." 

Mbali na kuwashukuru wanahabari, Nape pia amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua katika wizara hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na kusisitiza kuwa hana kinyongo chochote na Rais Magufuli kwa kuwa hata wakati wa uteuzi, hakuomba kuteuliwa, isipokuwa Rais alimteua kwa utashi wake licha ya kuwepo kwa watu wengi waliokuwa wakihitaji nafasi hiyo.

"Lengo langu kwanza ilikuwa ni kumshukuru Rais kwa uamuzi alioufanya pamoja na kwa kuniamini kwa mwaka mmoja,...Mimi Nape sina kinyongo na uamuzi wa Rais wangu, sina sababu ya kuupinga uamuzi wake... Nawaomba muungeni mkono Rais Magufuli, huyo ndiye Rais tuliyenaye, ndiye Rais tuliyepewa na mwenyezi Mungu" Amesema Nape

Amewataka watanzania kuendelea na maisha badala ya kukomaa na yeye, kwa kuwa yeye si mkubwa kuliko Tanzania huku akiwaasa vijana wa Tanzania kutokuwa waoga katika kusimamia kile wanachokiamini

"Tusihangaike na Nape, tuhangaike na Tanzania, Nape ni mdogo sana kuliko nchi. Tusije tukamgeuza Nape akawa mbadala au mkubwa kuliko Tanzania, Tanzania ni kubwa kuliko Nape... vijana wenzangu hamna cha kuogopa, simamieni mnachokiamini. ,.... Hatuna cha kuogopa isipokuwa uoga wenyewe."  Amesema Nape

Waziri Nape akiongea na RPC Kinondoni Suzan Kaganda, mara baada ya kuongea na wanahabari

VARANGATI

Awali, kabla Waziri Nape hajazungumza na wanahabari waliokuwa wakimsubiri ukumbini, palitokea varangati na vuta nikuvute baada ya kuwasili nje ya ukumbi, ambapo kulikuwa na taarifa kuwa mkutano huo na wanahabari umezuiliwa.

Kufutia taarifa hizo, baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni maafisa usalama walionekana kumzuia Nape kushuka ndani ya gari, lakini mwenye alikataa na kushuka kwa lazima hali iliyozusha vuta nikuvute, ambapo wangine walikuwa wakimzuia kuzungumza huku waandishi wa habari wakilazimisha azungumze hata akiwa hapo hapo nje ya ukumbi.

Baada ya Nape kupata mwanya wa kuzungumza, alieleza kukerwa na kusikitishwa na kile alichodai kuwa ni kuoneshwa bastola akilazimishwa kutozungumza kitu, huku akiwataka maafisa usalama kutokuwa na hofu kwa kuwa hakwenda pale kwa lengo la kuzungumza kitu kibaya.

Nape kwa jazba alisikika akisema "Yuko wapi yule aliyenioneshea bastola, namtaka aliyeinua bastola hapa, aje aeleze nani kamtuma na kwanini ameinua bastola......, kwanini tunahangaika na Nape.... mnatakiwa kujua kuwa nyinyi mnalipwa kwa kodi za wananchi.... kwani kuna jambo gani baya nimekuja kuzungumza hapa"