Jumatatu , 23rd Oct , 2017

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, William Lukuvi ameweka wazi mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli kwamba yupo radhi kufanya dhambi ya kuvunja nyumba za watu waliovamia kwenye eneo la mtanzania mnyonge ili eneo lirudi kwa

muhusika halali.

Waziri Lukuvi amebainisha hayo leo Ikulu Jijini Dar es salaam, baada ya Rais Magufuli kumaliza kuwapatia vyeti wanakamati waliofanya mazungumzo na kampuni ya Barrick Gold na wale waliofanya uchuzi wa thamani katika makinikia.

Amesema kwamba serikali haitawafumbia macho wavamiaji ambao wanawaonea wamiliki halali wa ardhi kwakuwa wao hawana pesa za kupambana nao kwa sababu wakati anakabidhiwa nafasi ya kuongoza wizara hiyo Mh. Rais alimuambia aende akawasaidie wanyonge.

Nitafanya dhambi ya kuvunja nyumba ya yule aliyevamia eneo la mwingine ili haki kamili irudi kwa mmiliki halali. Nilipokuwa Sumbawanga juzi Mbunge aliniambia viongozi wote wa Mkoa wameshindwa. Watu wababe wanatokea na kujenga kwenye viwanja vya watu maskini wale walio na hati ya umiliki. Serikali haitawafumbia macho wavamiaji kuwaonea wenye umiliki.

"Uliniambia niende wizara ile nikaondoe uonevu, kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria. Nipo kuhakikisha uonevu unakoma. Lazima nyumba zao tuziwekee alama ya X na tutazivunja. Lazima masikini wapatiwe haki zao. Japo najua changamoto ni nyingi na kwenye hii wizara kama unavyojua utajiri upo nje nje kwa sababu ya dhuluma niwaambie hatutawavumilia. Serkali tutasimama kuondoa ulaghai na wale wenye kujenga kwa kutumia mabavu tutawaondoa". Lukuvi

Ameongeza "Sitawafumbia macho watakaopora viwanja halali vya maskini kwa kuwa wao wanapesa, tutazivunja nyumba zao na miliki itarudishwa kwa mwenye nayo".