Jumatatu , 29th Mei , 2017

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha 'The United Democratic Party' (UDP) ametangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai ya kujipa fursa ya kuitumikia familia yake.

John Cheyo (Kushoto) akiwa na Goodluck Ole Medeye

Ole Medeye ambaye alijiunga na UDP akitokea CHADEMA mapema mwaka jana, ametoa kauli hiyo leo katika barua aliyomuandikia Mwenyekiti wa chama hicho Mh. John Cheyo, huku akimshukuru kwa kumuani katika nafasi hiyo kwa kipindi chote.

"Napenda kukujulisha rasmi kwamba ili nipate muda wa kutosha kufanya shughuli za ustawi na maendeleo ya familia na jamii inayonitegemea nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi hiyo ya Katibu Mkuu kuanzia tarehe ya barua hii".Imesema sehemu ya barua hiyo

Mwanasiasa huyo amewahi kushika nyazifa mbalimbali ikiwemo Ubunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi kupitia CCM katika Bunge la 10 na kupitia nafasi hiyo aliweza pia kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika serikali ya awamu ya nne.

Mara baada ya kushindwa katika kinyang'anyiro cha ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliamua kuhama chama na kujiunga na CHADEMA ambapo hakudumu sana licha ya CHADEMA kumpa nafasi ya kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha alihamia UDP kabla ya kupewa nafasi ya Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho.