Jumanne , 17th Jan , 2017

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole amefunguka na kusema kuwa wanasiasa wa vyama vingine ambavyo siyo CCM wamekuwa na juhudi kubwa ya kuwachonganisha wananchi na kuwafitinisha na serikali.

Humphrey Polepole

 

Humphrey Polepole amesema hayo leo na kutoa wito kwa wananchi na kuwataka wawapuuze wanasiasa wanaotumia matatizo na majanga kuwa mtaji wao kisiasa kwani serikali ipo kwa ajili ya kuwahudumia.

"Wanasiasa wa vyama ambavyo si CCM wamekuwa na juhudi kubwa kufanya uchonganishi na kuifitinisha serikali na wananchi, tunatoa wito kwa wananchi kuwapuuza wanasiasa wanaotumia matatizo na majanga kuwa mtaji wao kisiasa, Serikali ipo ili kuwahudumia. Siasa yetu ni ya Ujamaa na Kujitegemea, tutaendelea kuhimiza Watanzania kujitegemea na kuongeza juhudi katika kazi" alisema Humphrey Polepole

Polepole amesema CCM haitashiriki malumbano yasiyo kuwa na tija kwa lengo la kuleta uchochezi kwa wananchi kama ilivyo kwa viongozi wa vyama vingine nchini ambao wamekuwa wakitoa matamko kuwa taifa limekumbwa na baa la njaa kama sehemu yao ya mtaji wa kisiasa, jambo ambalo CCM kinaona hiyo ni siasa chafu.

Amesema mwenye mamlaka ya kutangaza baa la njaa nchini ni Rais pekee, hivyo ni vema wananchi wakajua kuwa Tanzania hatujafikia kiwango hicho cha njaa, bali wanatakiwa kujua kuwa hadi sasa tuna kiasi cha tani milioni 1.5 ambacho kitasambazwa katika maeneo mbalimbali ambayo yana upungufu wa chakula.

Aidha amesema mageuzi makubwa yanayoendelea ndani ya CCM yanalenga kukiimairisha Chama kuisimamia Serikali na kushughulikia matatizo ya watu