Ijumaa , 9th Apr , 2021

Mbunge wa kuteuliwa na rais Humphrey Polepole amesema ili kukuza masoko kwa wakulima inabidi yafanyike mageuzi makubwa ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kumuunganisha mkulima moja kwa moja na masoko.

Mbunge wa kuteuliwa na rais Humphrey Polepole

Polepole ameyasema hayo leo Jijini Dodoma akiwa bungeni wakati akichangia hoja ambapo amesema wakulima wanazalisha mazao yao kila siku hivyo Tanzania haina tatizo la uzalishaji wa mazao bali kunatatizo la masoko.

"Hapa Tanzania hatuna tatizo la uzalishaji, wakulima wanalima mazao kila mwaka kinachotakiwa sasa hivi nikutumia mageuzi makubwa ya Kitehama kumuunganisha mkulima moja kwa moja na soko na kuondoa ukiritimba wa madalali," amesema Polepole.

Pia ametoa raia kwa serikali kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo na wakati kwani ndio wenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi katika nchi.

"Biashara ndogo ndogo, na za kati ndio zinachukuwa asilimia kubwa ya chumi nyingi Ulimwenguni, ushauri wangu kwenye mpango tujikite kwenye kuwezesha biashara hizi kwani ndio injini ya uchumi wowote," amesema Polepole.