Jumatano , 27th Jul , 2016

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limezuia maandamano yaliyopangwa kufanywa na wanasheria na mawakili wa kujitegemea mkoani humo kupinga kitendo cha mwanasheria mwenzao kukamatwa na polisi kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kutoka kwenye mtandao.

Mawakili na Wanasheria wakiwa wanaandamana Jana jijini Arusha

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, amesema wamezuia maandamano hayo kutokana na kutokuwa na kibali cha polisi, ambapo amesema wakili huyo alikamatwa kwa taratibu za kisheria na kuachiwa kwa dhamana hivyo hakukuwa na sababu ya maandamano hayo.

Kamanda Ilembo, amesema kuwa mwanasheria huyo Shilinde Ngalula ambaye alikamatwa na Polisi Ngorongoro mnamo tarehe 25 mwezi huu, hivyo akawataka wanasheria hao kufuata taratibu zinazojulikana kufikisha malalamiko yao.

Aidha Kamanda Ilembo amewaomba wananchi, taasisi na wanasheria kufuata taratibu za kisheria wanapokuwa na jambo linalohitaji utatuzi wa pamoja ili kuepuka vurugu zinazoweza kujitokeza kutokana na maandamano hayo.

Pia ameziomba taasisi zinazoshirikiana katika kusimamia na kutafsiri sheria kushirikana kwa karibu ili kuwa mfano kwa jamii ili kudumisha utawala wa sheria.

Akizungumzia lengo la wao kukutana Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Mkoa wa Arusha, Modest Akida, amesema kitendo cha kukamatwa kwa wakili mwenzao ni kinyume cha taratibu za utawala wa kisheria jambo lililowalazimu kupeleka malalamiko yao kwa kamanda wa polisi.

SAUTI YA Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Mkoa wa Arusha, Modest Akida