Jumanne , 17th Oct , 2017

Muungano wa Upinzani nchini Kenya NASA umeahirisha maandamano yake dhidi ya tume ya uchaguzi nchini humo IEBC huku kukiwa na madai ya maafisa wa polisi kutumia nguvu zaidi dhidi ya waandamanaji ikiwa ni pamoja na kuua raia wasio na hatia.

Kiongozi wa upinzani nchini humo Bw. Raila Odinga amesema hatua hiyo imeafikiwa kufuatia vifo vya baadhi ya wafuasi wake ambao alidai walipigwa risasi na polisi na kuongeza kwamba muungano huo utatoa mwelekeo wake baada ya siku ya Mashujaa itakayofanyika Ijumaa .

Katika taarifa hiyo ya Odinga inadaiwa kumlaumu Waziri wa Usalama Fred Matiangi na Inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet akiwashutumu kwa kuwaagiza maafisa wa polisi kuua raia wasio na hatia.

"Kwa heshima ya wale waliouawa na serikali, maandamano yetu yataahirishwa. Siku ya Ijumaa tutawakumbuka raia wasio na hatia kama mashujaa kwa harakati dhidi ya haki ya uchaguzi katika eneo ambalo tutalitaja baadaye. Siku hiyo tutatangaza hatua tutakayochukua'', alisema kiongozi huyo wa upinzani.

Nasa, imesema inawataka maafisa wa polisi kusitisha mauaji hayo ambayo wamedai kuwa ni gharama kubwa kwa taifa.

''Serikali lazima isitishe ushirikiano wa maafisa wa polisi na majambazi mbali na ukiukaji wa kikatiba wa kuwapeleka polisi kuwakabili wafuasi wa NASA'', alisema.

Mapema leo Jumanne , Mahakama kuu ilisitisha kwa muda katazo la serikali dhidi ya maandamano ya IEBC katikati mwa miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu.
.