Jumanne , 20th Jun , 2017

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amewaonya wanaojihusisha na vitendo vya mauaji wilayani Kibiti na Rufiji, mkoani Pwani, huku akisema kuwa vitendo hivyo ndivyo vinafanya maeneo hayo kukosa kiwanda hata kimoja.

Ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Pwani Mhe. Magufuli amesema kwamba watu wanaochelewesha maendeleo ya Wilaya ya Kibiti na Rufiji ni wananchi wenyewe ambao wanawaficha watu wanaofanya uhalifu ilhali wanaishi mitaani kwao.

"Tunaochelewesha maendeleo ya Kibiti na Rufifi ni sisi wenyewe, kwa sababu tunawaficha watu wanaofanya vitendo vya kihalifu na mauaji, tuna kaa nao na tunawajua huku wengine wakiwa ni watoto wetu, tumewaficha kwa hivyo mtaendelea kukaa bila kiwanda hata kimoja. Lakini niseme watanyooka na salamu ziwasifikie. Serikali ya awamu ya tano siyo ya kuchezewa na watanyooka hata hivyo wameshaanza kunyooka. Hawatapita na nimesema hawapiti", alisema Rais Magufuli.

Aidha pamoja na hayo Rais Magufuli  amesema atahakikisha anazitatua changamoto zinazosababishwa na viongozi ambao wana tamaa na wanatumia vibaya rasilimali za nchi kwa kuwachukulia hatua viongozi wazembe wanaorudisha maendeleo nyuma.

“Niwahakikishie ndugu zangu kuwa nitalala nao mbele kwa nguvu zangu zote. Nitalala nao mbele kwa kumtanguliza Mungu ili maisha ya Watanzania yabadilike” Mhe. Magufuli aliongeza.