Jumatatu , 21st Aug , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa shirika la kimataifa la JICA Bw. Shinichi Kitaoka Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo amepongezwa kwa harakati za kupamabana na rushwa.

Katika mazungumzo hayo Bw. Kitaoka amempongeza Rais Dk. Magufuli kwa uongozi mzuri na wa mfano hasa msukumo mkubwa anaoutoa katika maendeleo hususani katika kuifanyaTanzania nchi ya viwanda pamoja na kupambana na vitendo vya rushwa.na kuahidi kuwa JICA itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania.

Bw. Kitaoka ambaye ni mara ya kwanza kuitembelea Tanzania amemuahidi Rais Magufuli kuwa miradi yote ya nyuma na ya sasa inayotekelezwa na Tanzania na JICA itamalizika kwa wakati ikiwemo mradi wa Flyover wa Tazara unaoendelea kujengwa, mradi wa barabara ya Mwenge - Morocco yenye urefu a kilometa 4.3 na mradi wa ujenzi wa daraja la Gerezani.

Kwa upande wake mh Dk. Magufuli amemshukuru Rais huyo wa JICA kwa uamuzi wake wa kuja Tanzania na amemuhakikishia Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao Japan inautoa katika maendeleo ya Tanzania kupitia JICA.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Masaharu Yoshida, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa wakala ya barabara nchini Mhandisi Patrick Mfugale.