Alhamisi , 8th Dec , 2016

Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki na Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mke wa Mwanzilishi wa Taifa la Sudan ya Kusini Rebecca Nyandeng Garang de Mabior.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Mke wa Mwanzilishi wa Taifa la Sudani Kusini Rebecca Nyandeng Mabior Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

Baaada ya mazungumzo hayo,Mke huyo wa Mwanzilishi wa Taifa la Sudan ya Kusini Rebecca Mabior amesema yeye pamoja na ujumbe wake wamelazimika kufika nchini Tanzania kuonana na Rais Dkt Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika ya Mashariki kwa lengo la kumfahamisha hali halisi ya nchi ya Sudan ya Kusini.

Amemuomba Rais Dkt Magufuli na viongozi wenzake wajumuia ya Afrika ya Mashariki kulisaidia Taifa la Sudan ya Kusini kutafuta suluhisho la mgogoro unaolikabili taifa hilo na kurejesha amani.

"Tumefarijika kuwa hapa katika ikulu ya Tanzania na tuko hapa kumsihi Rais Dkt Magufuli kama Mwenyekiti wa jumuia ya Afrika ya Mashariki akishirikiana na viongozi wenzake wa jumuia hiyo kuona namna gani wanaweza kutusaidia ili Taifa la Sudani ya Kusini liwe Taifa lenye amani,hivyo hapa tunawakilisha vilio vya watu wa nchi yetu na kikubwa tunachokitaka ni Amani katika nchi yetu na hiki ndio kilio chetu"

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mke wa Mwanzilishi wa Taifa la Sudani Kusini Rebecca Nyandeng De Mabior mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam

 

Rais Magufuli kwa upande wake amewasihi viongozi na wananchi wa Sudan ya Kusini kutafuta njia muafaka ya kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani na ili kuepuka machafuko yanayosababisha mateso kwa wananchi wa Taifa hilo.

"Mama Rebecca hata mimi binafsi naumizwa na kile kinachoendelea katika nchi ya Sudani ya Kusini hivyo,ningezisihi pande zote zinazotofautiana kumaliza tofauti zao kwa amani kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa la Sudani ya Kusini"

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mabior Garang Mtoto wa Mwanzilishi wa Taifa la Sudani Kusini Hayati John Garang De Mabior Ikulu jijini Dar es Salaam