Jumatano , 26th Jul , 2017

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu amewataka vijana wa skauti nchini kutumia mafunzo wanayopata ndani ya chama hicho vizuri kwani ni nguzo bora katika ustawi wa jamii isiyojihusisha na ufisadi wala dawa za kulevya.

Samia amesema hayo wakati akifungua maadhimisho ya miaka 100 ya skauti Tanzania yaliyofanyika kitaifa mjini Dodoma na kutarajiwa kuhitimishwa Julai 28 mwaka huu.

Amesema kwa sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya mmong'onyoko wa maadili hivyo ni wajibu wa vijana hao kuhakikisha wanaisaidia jamii inayowazunguka ili kujenga Tanzania yenye vijana wazalendo na wachapakazi.

"Nakusudia kusema tukilelewa vizuri ndani ya skauti baadae hatuwezi kuwa na viongozi wasaliti, wavivu, wala rushwa wazembe au wezi kwa sababu chama cha skauti kilijikita kwenye makuzi ya vijana, ujasiri na uzalendo na ukakamavu" Mh. Samia

Hata hivyo Samia amewataka Wakuu wa Wilaya na Maafisa Ardhi kote nchini kuhakikisha wanatenga maeneo ambayo vijana hao watafanya shughuli za uzalishaji kama kilimo na mifugo ili kuwashawishi wananchi wanaowazunguka.

Kwa upande wake Rais wa skauti Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako amewataka vijana waliopo mashuleni na vyuoni kujiunga na vilabu vinavyoanzishwa mashuleni na kufanya kazi baada ya masomo ili kujiepusha na vishawishi hasa matumizi ya dawa za kulevya.