Jumanne , 21st Nov , 2017

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaagiza watendaji wa Tanesco kuhakikisha kuwa hawakati umeme bila sababu maalum na hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kukosa nishati hiyo.

Mh. Subira ametoa agizo hilo leo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa TEDAP unaohusu upanuzi na ujenzi wa vituo vya kupozea Umeme na njia za Umeme vya Mbagala, Gongo la Mboto, Kipawa na City Centre.

Amesema, umeme ukatike pale inapostahili tu, na endapo tatizo linatokea kwenye mifumo ya Umeme ni muhimu Tanesco ikatoa taarifa mapema kwa wananchi,na kwamba kukosekana kwa nishati hiyo kunaathiri shughuli nyingi hasa za kimaendeleo na kiuchumi zinazowaingizia kipato wananchi.

Aidha Naibu Waziri amewaagiza watendaji wa Tanesco wanaosimamia mradi huo wa TEDAP jijini Dar es Salaam, kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika tarehe 15 Desemba, mwaka huu.

Mradi wa TEDAP unahusisha upanuzi na ujenzi wa Vituo Vipya 19 vya kupoza Umeme wa Msongo wa kV 132/33 na kV 33/11 pamoja na ujenzi wa njia za Umeme wenye Msongo wa kV 132, kV 33 na kV 11 katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro na utagharimu Dola milioni 43 zilizotolewa na Benki ya Dunia .