Alhamisi , 22nd Jun , 2017

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya awamu ya tano haitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini mpaka hapo vitendo hivyo vitakapokoma.

Makamu wa Rais Samia Suluhu

Mhe. Samia ametoa kauli hiyo leo wakati anafungua Mkutano wa Kimataifa wa ngazi ya juu wenye lengo la kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya Rushwa katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa vita ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ni kipaumbele cha kwanza katika serikali ya awamu ya tano.

"Kupambana na rushwa ni jambo la msingi na muhimu kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu katika nchi yeyote duniani. Rushwa ni mbaya na imeharibu sana maisha ya watu, maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hivyo ni lazima ikomoshwe ili jamii iishi maisha mazuri na wale wote wanaounufaika au kuhusika na vitendo hivyo wataendelea kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo nchini. " alisema Mhe.Samia 

Vile vile, Makamu wa Rais amesema kuwa hakuna nchi yeyote ambayo haijaguswa na misukosuko ya vitendo vya rushwa duniani lakini Bara la Afrika limeendelea kuteseka sana na vitendo hivyo kwa miongo kadhaa hivyo jitihada za pamoja zinatakiwa katika kutokomesha vitendo hivyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa wizara yake itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali watumishi wa umma watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwenye maeneo yao ya kazi.