Jumatano , 13th Sep , 2017

Pamoja na kukiri kuwa watoto wa kike hupata tabu ya kujihifadhi mpaka kutumia majani wakati wa hedhi kutokana na kushindwa kugharamia taulo za kike (Pedi),  Waziri wa Afya,  Ummy Mwalimu amedai bado anasubiri majibu ya kuondolewa kodi za bidhaa hizo.

Waziri Ummy Mwalimu

Akijibu swali la Mbunge wa viti maalum Mh. Stella Ikupa aliyehoji kuhusu serikali lini itafanya maamuzi ya haraka kuhusiana na kodi zinazopelekea taulo za kike kuuzwa kwa bei ghali huku wanaoathirika wakiwa ni watoto wa kike wengi wasiokuwa na uwezo wa kugharamia hivyo kulazimika kutumia njia hatarishi kujihifadhi.

"Nikiwa kama Waziri wa Afya lakini pia ni mama mwenye watoto wa kike  nikiri kwamba changamoto katika jambo hili ni kubwa sana. Nakiri wapo wanafunzi wanaokosa masomo hata kwa siku tano kwa mwezi ili kujihifadhi kutokana na kutokuwa na taulo salama, lakini wapo wanaotumia mpaka majani.  Ombi la kuondoa kodi nimeshalipeleka kwa waziri wa fedha na hata sasa nilikuwa namtafuta humu ndani ili kumsihii aharakishe mchakato huu", amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Afya Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa maamuzi kuhusu kuondolewa kodi kwa taulo hizo yalishawasilishwa bungeni mara kadhaa lakini pia maamuzi kamili yamekuwa yakichelewa kutoka kutokana kuwa bidhaa hizo hazijawahi kuorodheshwa kama vifaa tiba.

Hata hivyo. Mh. Kigwangalla ameongeza kwamba mpaka sasa bidhaa hizo zimeshaondolewa ushuru kutokana na kuwa zina umuhimu mkubwa lakini pia majadiliano bado yanaendelea ili kodi yake iweze kuondolewa kabisa.

Mbali na hayo Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge wanawake kusimamia kuondolewa kodi katika taulo hizo za usafi za kike ‘pedi’ kutokana na kutozwa kodi kwani zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa hali inayowafanya wanawake wengi kushindiwa kumudu kuzinunua.

Amesema kodi hiyo imekuwa kero, hivyo amemtaka mwenyekiti wa wabunge wanawake, Magreth Sitta kubeba jukumu hilo.
Spika ametoa kauli hiyo kutokana na majibu ya Serikali kutoeleza moja kwa moja ni lini itaondoa kodi kwa taulo hizo.

Katika kumbukumbu mwezi Machi mwaka huu kuelekea siku ya Wanawake duniani Kampuni ya East Africa LTD pamoja na Hawa Foundation zilitumia siku hiyo kuendesha kampeni ya uchangiaji wa taulo za kike ambapo baadhi ya shule zenye uhitaji nchini Tanzania zilifikiwa kupata msaada huo.

Baadhi ya Matukio ya ugawaji na upokeaji taulo za kike zilizopatikana na kwenye kampeni ya Namthamini ya East Africa Tv na Radio